Alhamisi, 16 Oktoba 2014

KATLESI ZA NYAMA YA KUSAGA

Vinavyohitajika

Nyama  ya  kusaga robo kilo

Chumvi

Mbataa   8 za kiasi

Thomu na tangawizi  iliyosagwa

Pili pili  manga  kijiko  cha  chai

Bizari nzima iliyosagwa  nusu kijiko  cha  chai

Mayai  ya  kuchomea

Mafuta  ya  kupikia

Matayarisho

·         kausha  nyama  yako  na  viungo  vyote.
·         iwache  ipoe.
·         menya  mbatata  zako  uzichemshe   na  uziponde  zikisha  wiva(usisahau kutia chumvi unapozichemsha mbatata)
·         zisubiri   zipoe .
·         tengeneza  mviringo  wa  mbatata  ulizoziponda  na  uweke  nyama  yako  kati. 
·         izibe  nyama  yako kwa mchanganyo  wa  mviringo  wako  wa  mbatata  ulizoziponda.
·         teleka  chuma  chako  cha  mafuta  yawache  yapate  moto.
·         lipige  yai  lako  kwenye  kibakuli tia  chumvi  kidogo.
·         chovya  mviringo  wa  katlesi  yako  kwenye  yai  na  uanze  kuchuma.
·         yai  likiwiva  zitoe   na  uweke  kwenye  chujio  zijichuje   mafuta.
·         ukisha  maliza  weka  kwenye  sahani  tayari  kwa  kuliwa.

Kidokezo

 

Unaweza  kutia  kitunguu maji vidogo vidogo  kwenye   nyama  yako  pia  zina kuwa  nzuri.

Pia kotmiri  kwa  wanaopenda  na  hata  pilipili  pia.

Zikiwa  zinapasuka  unapozichoma  usisahau uzigaragaza  kwenye  unga  wa ngano kidogo  ukisha  ndio  uzichove  yai  na  tayari  kwa  kuchomwa

SHARUBATI YA EMBE

Vinavyohitajika

·         Maziwa  lita 2
·         Kibati  cha mango pulp kimoja au embe fresh iliyomenywa unayoweza kupata pulp.
·         Sukari  kiasi

Namna ya kutayarisha na kutengeneza

·         Mimina maziwa kwenye blender.
·         Pamoja na sukari na mango pulp.
·         Isage kwa pamoja  ichanganyike.
·         Imimine kwenye jagi na uweke barafu ya kutosha.
·         Tayari kwa kunywewa.

Kidokezo

Sharbati hii ni nzuri kwa afya na pia unaweza kuifanya kwa matunda tafauti uyapendayo lakini yasiwe ya ukali tu kwani maziwa yatakatika

BANZI ZA MAZIWA

Vinavyohitajika

Unga  wa  ngano  magi 3

Maziwa  ya   maji  magi  1

Hamira  vijiko  2 vya  kulia

Maji  kiasi

Chumvi kijiko 1  cha  kulia

Mafuta  ya  kupikia  au  siagi  vijiko  2 vya  kulia

Namna  ya  kutayarisha

Changanya  unga, hamira, chumvi pamoja  na  maziwa  vichanganye  pamoja.

Ongezea  maji  kidogo  kidogo  mpaka  uchanganyike  na  uuanze  kuukanda.

Ukande   vizuri  mpaka    ukandike   ulainike.

Chukua   tray  zako  upake  mafuta  na   ukate  madonge  ya  unga  upange  kwenye  tray  uwache  uumke   na  uchome  kwenye  oven  gas  mar  7  au  Jiko    la  umeme  200.

Kidokezo

Hakikisha  madonge   ya  unga yasiwe  makubwa  kama  ya   mikate   ya   kusukuma.

MIKATE YA UFUTA YA KIASILI


Vinavyohitajika

Nazi  kipande  1

Nnga  magi  4

Chumvi

Sukari  kijiko  1  ½  cha  chakula

Ute  wa  yai  1

Hamira  vijiko 3  vya  chakula

Ufuta  wa kutosha

Namna  ya  kutayarisha  na  kupika

·         iroweke  nazi  yako  kwenye  blender  kwa  maji  ya  vuguvugu  na  uisage  vizuri
·         weka  unga  wako   ndani  ya  bakuli  na  utie  hamira, chumvi ,sukari  na  ute  wa  yai
·         changanya  unga  wako  kwa  nazi  uliyokwisha  isaga  (tui)
·         upige  unga  wako   (tofauti  na  kuukanda) namaanisha  unga  huu unazidi  maji
·         ukisha  changanyika  vizuri   unga  wako  ufunike  na  usubiri  uumke
·         ukisha  umka
·         weka  bakuli  la  maji  na utie  chumvi  kiasi(lakini  ukiyaonja  chumvi ijitokeze)
·         weka  chuma  chako  kwenye  jiko  kipate  moto  rushia  maji  yenye  chumvi  kwenye chuma  cha  moto
·         teka  unga  wako  kwa kiganja  cha  mkono  una uutandaze  kwenye  chuma 
·         nyunyiza  ufuta  juu ya  mkate  wako  kabla  haujakauka
·         utie kwenye   grill  hapo  utaumuka  na  kuwiva  kuwa  rangi  nzuri  ya  kuvutia
·         rejesha  tena  juu  ya  jiko  kwa moto  wa kiasi  na  uupake  mafuta  kwa  brash 
·         utoe  na  uuweke  sahanini  tayari  kwa  kuliwa.

Kidokezo

Ukitia  yai  na kiini  chake  cha  manjano  utachelewa  kuumka  na  hautakuwa  na  rangi nzuri  ya   kuvutia

MSETO

Vinavyohitajika

·         Choroko zilizopaazwa magi 1
·         Nazi ya kipande ½ (cream coconut)
·         Mchele magi 1
·         Chumvi

Namna ya kutayarisha na kupika

·         Roweka choroko kwa muda wa masaa 2 kwenye maji ya vuguvugu.
·         Injika sufuria ya maji kwenye jiko na usubiri yachemke sawa sawa na uzigide maji choroko zako na uzitie kwenye maji hayo yanayochemka.
·         Pia roweka mchele  kwenye maji ya kawaida.
·         Choroko zikishawiva utaziona zimeachana kiasi cha kwamba ukizishika kwa vidole zinavurugika bila ya kutumia nguvu .
·         Gida maji mchele na umimine kwenye mchemko wa choroko.
·         Weka chumvi kiasi.
·         Isage nazi kwa kutumia maji ya vuguvugu na uhakikishe imesagika na kutoa tui lililokuwa zito kiasi cha 1/2 ya magi yako.
·         Irudie kuisaga tena nazi  kwa kipimo cha maji magi 1
·         Mchanganyiko wa mchele ukishawiva vizuri, weka tui la nazi  ya kipimo cha magi1.
·         Kifunike chakula mpaka maji yawe yamekauka na uanze kuusonga mseto ili upate kuchanganyika vizuri na uweke lile tui lako zito la mwanzo ambalo ni ½ magi. Usonge vizuri na upambie kwa muda wa dakika 10 na uupakue kwenye sahani na tayari kwa kuliwa.

Kidokezo

Mseto usiuwache ukauke sana kwa sababu kila ukikaa unazidi kujishika na kuwa mgumu kwani unapendeza kuliwa ukiwa mlaini kidog

Egg roll

Vinavyohitajika

1.   Nyama  ya  kusaga  ¼  kilo
2.   Mayai  4  makubwa
3.   Papi  za  sambusa  3
4.   Chumvi
5.   Pilipili  mtama (manga) ½  kijiko  cha  kula
6.   Pilipili  boga  ¼ 
7.   Kotmiri  ½  ya  kisahani  cha  chai
8.   Thomu  na   tangawizi  kijiko  1  cha  chai
9.   Ndimu  kijiko  1  cha  chai
10.                Unga  wa  toast (bread  crumble)
11.                Mafuta  ya  kupikia

Namna  ya  kutayarisha 

·         Katakata  pilipili boga  vipande  vidogo vidogo. 
·         Chambua  majani  ya  kotmiri .
·         Kausha  nyama  yako  kwa  kutia thomu na  tangawizi, pilipili manga,chumvi  pamoja na  ndimu.
·         Iwache  ipoe.
·         Piga  mayai  yako 3  kama  kiwanda  uyamimine  kwenye  chuma  cha  mafuta  ya moto (weka  kijiko  kimoja  na  nusu  cha  chakulia).
·         Tandaza  nyama  yako  ndani  kiwanda  na  utie   pilipili  boga  juu  yake  na ikifuatiwa  na  kotmiri.
·         Kigeuze  kiwanda  chako  upande  wa  pili  na   uhakikishe  kimewiva  vizuri.
·         Ukisha  maliza  kupika  kiwanda. 
·         Weka  kaki zako  kwa  mpangilio   ufuatao:-
1.   Weka  papi  yako  ya  kwanza  na  uipake  ute  wa yai  pembezoni.
2.   Na   weka  papi yako  ya  pili  juu   yake  zishikane.
3.   Paka  tena  ute  wa  yai  mwisho  wa  papi  zako  mbili
4.   Weka  kaki  yako  ya  tatu  mwisho  wa  kaki  yako  ya   pili  ili  zishikane  upate urefu  unaohitajika
·         Kiweke  kiwanda  chako  juu ya  kaki  zako  mbili  ulizounganisha  mwanzo.
·         Anza  kuroll  mpaka  mwisho  na  hakikisha  unapata  mviringo  uliokaa  sawa.
·         Tayari  kwa  kukata  slice  za  mviringo  huo.
·         Paka  mviringo  wako yai  pembeni.
·         Ugaragize  kwenye  unga  wa  toast.
·         Anza  kuzichoma  egg rolls  zako  kwa  moto mdogo mdogo   kwenye  chuma cha   kuchomea  lakini  usiweke  mafuta  mengi  ( weka  vijiko  vya  chakula  4 vya  mafuta  kwa  kila  egg roll  8).

·         Vitowe  na  tayari  kwa  kuliwa

Kidokezo

Ni vizuri  kuhimiza  kuvikata wakati  yai  likiwa  limoto  na  kaki  kabla  ya  kukauka  kwani ukichelewa  utapata  tab

Keki ya kawaida

Keki ya Kawaida
 
Vinavyohitajika

·         Siagi ya baking 500g – nusu kilo.
·         Sukari 500g – nusu kilo.
·         Unga  wa ngano 1000g – kilo moja.
·         Arki rose kijiko 1 cha kulia chakula.
·         Arki vanilla kijiko 1 cha kulia chakula.
·         Baking powder vijiko 2 vya kulia chakula.
·         Cocoa au unga wa kahawa vijiko 3 vya kulia chakula.
·         Unga wa mdalasini kijiko 1 cha chai.
·         Mayai yakiwa makubwa 10 na yakiwa madogo 12.
·          Baking tray - Tray ya Kuokea.

namna  ya kutayarisha

·         Weka siagi ndani ya bakuli la kuchanganyia  pamoja na sugari  uichanganye  pamoja mpaka vichanganyike  vizuri (unaweza kuisaga  sukari yako ukitaka lakini si lazima).
·         Ikichanganyika vizuri weka mayai uchanganye pamoja pia  ichanganyike  vizuri.
·         Weka arki zote mbili kwa pamoja huku  ukizichanganya
·         Uchanganye unga na baking powder na uanze kuweka kwenye mchanganyiko wa siagi, mayai  na sukari.
·         Hakikisha unaweka unga wako kidogo kidogo na sio wote kwa wakati mmoja.
·         Ukisha changanyika punguza  mchanganyiko huo robo yake kwenye bakuli jengine na utie unga wa Cocoa au kahawa pamoja na mdalasini na uchanganye  vizuri mpaka ubadilike uwe rangi moja.
·         Ipake  siagi  kwenye baking tray na umimine mchanganyiko wa keki  ambayo haina cocoa robo ya unga na utandaze vizuri.
·         Weka mchanganyiko wako wenye cocoa juu yake pia utandaze vizuri.
·         Malizia kwa kuweka mchanganyiko wa keki iliyokuwa haina cocoa kwa juu tandaza vizuri na tayari kwa kuichoma.
·         Kwa wanaotumia jiko la Gesi ni kipimo cha mark 5 na kwa wale wanotumia jiko la umeme ni mark 250 ya spidi ya jiko.
·         Ili iwive vizuri na kuwa na rangi ya kupendeza inachukua muda wa saa 1  kuokwa na tayari kwa kuliwa.

Kidokezo

Unaweza kutumia mashine ya kusagia keki na kama huna  tumia mwiko tu kwa kuchanganyia na itakuwa nzuri tu usikhofu. Pia isubiri keki  ipoe ndio uitowe kwa kuhofia isije ikakatika wakati wa kuitoa kwenye  tray ya kuokea - baking tray.

UROJO

Mbatata za Urojo

 
 
Vinavyohitajika

Mbatata  ¼ kilo

Bizari ya manjano ¼ kijiko cha chakula

Ndimu 1 kubwa

Embe mbichi moja

Chumvi

Unga wa ngano vijiko vya chakula 4

Namna ya kutayarisha na kupika

Chemsha mbatata na maganda yake

Zikishawiva, ziepue na uziwache zipoe

Teleka sufuria ya maji kwenye jiko lenye moto pamoja na embe mbichi

Koroga unga kwa maji na bizari uwe kama wa kupikia uji

Maji yakianza kupata moto weka unga na upike kama uji

Uwache uchemke na huku ukiukoroga

Kamua ndimu uweke kwenye urojo pamoja na chumvi

Zimenye mbatata na uzikate vipande vidogo vidogo uweke kwenye bakuli na umimine urojo tayari kwa kuliwa.

Kidokezo

Zinapendeza kuliwa kwa mishikaki ya kuku au nyama. Pia bajia ndio mwenziwe pia usikose chips za muhogo na kachori.

Jumatatu, 29 Septemba 2014

BIRIANI YA SAMAKI

MAHITAJI:

Mchele 1kg

Samaki 1kg

Vitunguu maji 1kg

Samli kiasi

Thomu

Mmdalasini

Hiliki

Ndimu

Nyanya

Chumvi kiasi

Njia:

1. Mkatekate samaki umtie chumvi ndimu umkaange. Menya vitunguu
uvikate. Saga nyanya. Thomu na viungo vyote vilivyosalia. (bakisha
mdalasini nzima kidogo)

2. Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange,
vikianza wekundu tia nyanya na viungo kidogo. Acha vikaange kwa
muda mdogo halafu tia vipande vyote vya samaki, chumvi na ndimu,
pamoja na maji kidogo. Acha ichemke kwa muda mdogo ibaki na rojo
rojo epua.

3. Chukuwa sufuria nyengine uitie maji na chumvi. Yakichemka osha mchele
utie. Acha utokote. Angali kiini wali. Ukiona umewiva umimine uyachuje
maji yote. Teleka tena sufuria pamoja na vile viungo ulivyovisaga. Vyote
vikaange kidogo halafu umimine wali wote ukorogekoroge ili upate
kuchanganyika na viungo. Halafu uweke vizuri upalie moto. Ukishakauka
utaupakuwa. Kuupakuwa kwake utatia wali sahani, baadae ndio utatia
samaki pamoja na rojo rojo zake kwa juu.

VILEJA VYA CHUMVI

MAHITAJI:

Siagi *

Unga wa ngano 1kg

Mayai 2

Jam

Njia:

Changanya unga na siagi mpaka uchanganyike sawa sawa, kama mgumu tia
maji baridi kidogo. Kata nakshi uipendayo huku ukipaka yai na jam juu yake.
Choma na wacha vipoe.

TOFI

MAHITAJI:

Maziwa ya kibati

Maji * kikombe

Hiliki

Sukari na arki kiasi

Njia:

Teleka maziwa changanya maji, sukari arki na iliki koroga usiwache mkono
mpaka iwe nzito. Tia samli kidogo na epua. Tandaza kwenye sinia
iliyopakwa samli na kata.

FARNE


MAHITAJI:

Unga wa mchele

Maziwa yaliyochemshwa

Iliki na sukari

Njia:

Teleka maziwa na yakichemka tia sukari na iliki wacha yachemke tena
kidogo. Tia unga uliovurugwa kwa maji na wacha uchemke kidogo. Ukiwiva
epua na mimina ndani ya bakuli. Wacha ipoe na kata vipande. Tayari kwa
kula.

VIKONI

MAHITAJI:

Unga wa ngano

Pilipili manga

Chumvi

Siagi

Nyama ya kusaga iliyochemshwa na kutiwa viungo.

NJIA :

Changanya unga na samli, chumvi na pilpili manga mpaka vichanganyika na
kua kitu kimoja kata madonge na sukuma kwenye kibao.Kata kwa umbo la
duara na weka nyama yako katikaati. Pasua kidogo kwa kisu pinda duara na
ikae kama koni na nyama itokeze juu. Choma kwa oven au kwa makaa na
vikikaribia wekundu epua.

KITAWA


MAHITAJI:
Ndizi mbichi 6

Chumvi

Maziwa ya mgando

Njia:

Menya ndizi na kata vipande vifupi. Safisha ndizi vizuri hadi utomvu utoke,
kisha zichemshe hadi zilainike vizuri, ziponde kisha zichanganye na maziwa
ya mgando hadi kuwa kama uji mzito. Pakua na andaa.

KARI YA SAMAKI

MAHITAJI:

Mnofu wa samaki4oz

Nyanya 1

Kitunguu maji

Thomu

Bizari

Limau

Maziwa fresh

Mafuta ya maji.

NJIA

Safisha samaki na kata vipande.Menya na katakata vitunguu,na ponda
vutunguu thomu.Osha na menya nyanya ikate vipande vidogovidogo. Pasha
moto mafuta na kaanga vitunguu. Ongeza viungo vyengine na endelea
kukaanga. Ongeza nyanya na endelea kukaanga, zikilainika ongeza samaki
na maziwa na endelea kupika taratibu kwa muda wa dakika 10-15. Ongeza
maji ya limau na endelea kutokosa kwa dakika 3 zaidi. Epua na andaa.

VICTORIA SANDWICH

MAHITAJI:

Unga wa ngano 6oz

Mayai 4

Jam vijiko vya mezani 2

Siagi 4oz

Chumvi mziwa kidogo.

Njia:

Saga mchanganyiko wa sukari na siagi hadi uwe laini na mwepesi kidogo,
pasua mayai na pigapiga na ongeza kwenye mchangayiko kidogo kidogo.
Chekecha unga, chumvi na changanya kwenye mchangayiko kidogo kidogo.
Ongeza maziwa hadi mchangayiko uwe mweupe kidogo (unaomiminika) Paka
mafuta legeni 2 na weka mchanganyiko wa keki kwenye legeni zote. Oka
kwa dakika 20 kwenye oven.

Keki ikiiva epua na acha ipoe. Paka jam juu ya keki moja sehemu ya chini na
shikamanisha na keki ya pili. Nyunyiza sukari laini juu au pamba
upendavyo.

LEMON BISCUITS

MAHITAJI:

Unga wa ngano 4oz

Siagi 2oz

Kiini cha yai 1

Sukari 2oz

Ganda la limiau lililokunwa.

Njia:

Paka legeni mafuta, chekecha unga na fikicha siagi hadi mchanganyiko
ufanane na chenga za mkate. Ongeza sukari na ganda la limau. Ongeza kiini
cha yai lililopigwa, ongeza na maji baridi kidogo hadi kiwe laini na kufaa
kusukumwa, sukuma kinyunga hadi kiwe na unene wa 3 kata mviringo ya
biscuits na weka kwenye legeni. Toboa mashimo ya urembo oka biskuti
kwenye oven zikiwiva epua na nyunyiza sukari ukipenda.

PAI YA NYAMA


MAHITAJI:
Nyama ya kusaga oz 6

Karoti 1

Kitunguu 1

Nyanya 1

Giligilani 2tsp

Chumvi 1 tsp

Yai lililopigwa

Maziwa 2oz

Siagi 2tsp

Viazi mviringo vilivyopikwa na kupondwa 6oz.

Njia:

Pika nyama hadi iwive, Menya kitunguu na karoti na kata vipande vidogo
vidogo. Menya nyanya na katakata, pasha mafuta moto na kanga viungo
vyote, ongeza nyama na maji kidogo visiwe vikavu sana, Ponda viazi vingali
moto ongeza siagi, maziwa na chumvi, Paka mafuta chombo cha kuwekea
pai (pai dish) na weka mchanganyiko wa nyama ndani. Tandaza viazi juu ya
nyama. Sawazisha kwa kisu. Tengeneza viumbo lolote juu ili kupamba. Paka
yai juu ya viazi kisha oka kwenye oven yenye joto 160deg C. hadi pai iwe
kahawia. Epua na andaa pamoja na mchuzi rojo. N.B. unaweza kupaka
maziwa juu badala ya yai.

PAI YA SAMAKI

MAHITAJI:

Samaki oz 12 (minofu iliyochemshwa)

Viazi vidogo 3 vilivyochemshwa

Nyanya ndogo 3

Macaroni oz 2, (yaliyochemshwa na kupakwa siagi, chumvi, Jimbini 2 oz

Pilipili ya ungaa * tsp

Siagi oz 1

Mayai 2

Maji yaliyochemshiwa samaki * kikombe

Chenga za mkate oz 1.

Njia:

Paka mafuta kidogo, piga piga mayai ndani ya bakuli na ongeza minofu ya
samaki yalichambuliwa na nusu ya viazi vilivyopondwa, chumvi, pilipili na
macaroni, ongeza mchuzi wa samaki na changanya vizuri. Pakua nusu ya
mchanganyiko ndani ya pie dish. Panga nyanya zilizokatwa slice za * ikisha
ongeza mchanganyiko uliobaki na panga tena nyanya zilizobaki. Funika na
mchanganyiko wa viazi vilivyobaki.

Nyunyiza jibini na chenga za mkate juu ya pie kisha paka (dondosha) siagi
kidogo kidogo juu yake. Oka katika oven yenye joto 125-150 deg.C. mpaka
pie iwive na iwe rangi ya kahawia epua.

FISH ROLL

MAHITAJI:
Samaki 2 wabichi waliochemshwa

Viazi mviringo vilivyochemshwa na kupondwa

Siagi tsp 1

Yai lililopigwa

Chenga za mkate

Maziwa fresha 2tsp

Chumvi 1 tsp

Chumvi 1tsp

Pilipili ya unga

Njia:

Ondoa ngozi na mifupa kwenye samaki na chambua minofu. Ongeza viazi
vilivyopondwa na siagi, ongeza pili pili na chumvi, ongeza nusu ya yai na
changanya vizuri kama mchanganyiko ni mkavu ongeza maziwa, changanya
vyema na tengeneza mviringo mirefu 4, pakaza yai lililobakia na viringisha
samaki (rolls) kwenye chenga za mkate. Paka legeni mafuta na kuoka rolls
kwenye oven na joto 170 – 180 degrees F. kwa muda wa dakika 20 – 25.
andaa pamoja na tomato sauce.

N.B waweza kukaanga rolls kwenye mafuta (kwa kutosa) hadi iwe rangi
kahawia na hudhurungi baada ya kuokwa.

MEAT CURRY

MAHITAJI:

Nyama oz 8

Bizari oz 1

Vitunguu 3 vilivyolengwa

Pilipili 1

Thomu tembe 2

Tangawizi iliyosagwa

Mafuta ya maji oz 2

Nazi1

Limau1/4.

Njia

1. Safisha nyama na kata vipande vidogovidogo.

2. Ongeza kitunguu thomu, thangawizi na bizari kwenye nyama
changanya vizuri iwache kwa muda viungo vikolee.

3. Kamua na chuja tui la nazi mara tatu.

4. Pasha moto mafuta na kaanga vitunguu hadi viwive, Ongeza vitunguu
na nyanya na endelea kukaanga kwa dakika2

5. Ongeza tui la nazi ulilokamua mara ya pili na tatu changanya vizuri
na koroga na acha ichemke.Ongeza tui la kwanza,punguza moto na
kuacha nyama iendelee kutokota.

6. Epua na ongeza kijiko kidogo cha maji ya limau koroga vuzuri na
andaa.

Kari ya nyama yaweza kuandaliwa na wali au mkate.

SAMAKI WA KUKAANGA

MAHITAJI:

Minofu 2 ya samaki mbichi

Yai 1 piga

Chumvi kiasi

Mafuta

Maji tbl sp 2

Chenga za mkate tb. Sp 2

Njia :

1. Osha minofu ya samaki ikaushe maji na ipake chumvi na pilipili.

2. Weka vipande vya samaki kwenye yai na vibinginishe kwenye
chenga za mkate.

3. Kaanga minofu ya samaki hadi iive na ibadilike rangi ya kahawia.epua
andaa

DINNER ROLL

DINNER ROLLS

Unga wa ngano 8oz

Sukari tsp 1

Siagi 1oz

Chumvi tsp1

Hamira tsp 1

Maziwa ya uvugu uvugu kikombe 1

Yai 1

Njia:

Chekecha unga na chumvi kwenye bakuli kubwa

Fikicha siagi na unga

Tengeneza shimo katikati ya unga na tia sukari na hamira. Changanya ili
kufanya uji mwepesi sana. Funika na weka mahali pa uvugu uvugu kwa muda
wa dakika 10-15.

Hamira ikisha umuka changanya unga na maziwa au maji ya uvugu na fanya
kinyunga kanda kiunga vizuri na bila kuongeza unga ikiwezekana.

Acha kinyunga kiumuke mara mbili ya ukubwa wake kisha kanda tena.

Tengeneza maumbo mbali mbali kisha acha ili uumuke tena weka kwenye
legeni.

Piga piga yai kisha paka juu ya rolls oka kwenye oven yenye joto 300F –
350F au 170C – 180C kwa muda wa dakika 15-20 epua.

JAM BUNS

JAM BUNS/ANDAZI LA JAM

Unga wa ngano 8oz

Hamira ya unga vijiko vya chai tsp2

Mayai 2

Jam vijiko vya kulia 2

Siagi vijiko vya kulia 2

Sukari vijiko vya kulia 4

Maziwa * kikombe

Njia:

Chekecha unga na hamira kwenye bakuli kubwa

Fikicha siagi na unga hadi mchanganyiko ufanane na chenga za mkete.

Ongeza sukari na changanya vyema.

Ongeza yai lililopigwa mara 2 na maziwa na changanya vyote vizuri ili kuwe
na donge laini. Washa oven 250F-300F au 140C-150C.

Tengeneza shimo katikati ya kinyunga kwa kidole na weka juu jam kidogo.

Tengeneza vimviringo vidogo vidogo kwa kiganja cha mkono.

Paka mafuta legeni na weka vile vimviringo kwenye legeni.

Oka kwenye Oven kwa muda wa dakika 15 – 20

Epua na tayarisha

MEAT CAKE

MEAT CAKE

Nyama 11/2kg (ya kusaga)

Siagi 1/4kg

Unga1/4kg

Carrot1/4kg

Pilipili mbuzi 1/4kg

Mayai 18

Uzile

Mdalasini

Pili pili manga

B.powder 2tsp

Ndimu 1

Thomu kidogo

Method:

Changanya nyama, thomu, ndimu, pilipili manga, mdalasini na uzile na upike
pamoja iwive kasha saga siagi na mayai 6 hadi iwe cream na nyepesi kama
unavyofanya kwa keki ya sukari kasha changanya pamoja kwa unga na
B.powder changanya kwa mkono mpaka uchanganyike piga mayai mengine 6
na uchanganye na ile nyama kwa kijiko mpaka ichanganyike vizuri. Para
carrot zako kwa kutumia kile kibati cha kuparia chips nazo ziwe kama chips
tena zichemshe kidogo ziwive, kata pilipili boga ziwe slices za duara
nyembamba. Mwisho paka trey yako siagi itandaze ienee yote na mimina ule
mchanganyiko wa cake juu yake halafu tandaza juu yake ule mchanganyiko
wa nyama na mayai, tena vunja mayai 6 yalibakia uyapige vizuri, tandaza
carrots zako juu yake na zile slices za pili pili boga, kasha malizia kwa
kunyunyiza mote yale mayai uliyoyapiga tia ktk oven pre-heated temp. 180C
mpaka ikauke na iwive na ikipoa kata square na uwandae.

Jumapili, 28 Septemba 2014

HALF CAKE

Mapishi ya Half cake (Keki)

Mahitaji
Unga wa ngano (self risen flour) kikombe 1na 1/2
Sukari (sugar) 1/4 kikombe
Barking powder 1/2 kijiko cha chai
Magadi soda (bicarbonate soda) 1 kijiko cha chai
Mafuta 2 vijiko vya chai
Mafuta ya kukaangia
Maji ya uvuguvugu kiasi

Matayarisho
Changanya unga na vitu vyote (kasoro mafuta ya kuchomea) kisha ukande (hakikisha unakuwa mgumu) Baada ya hapo sukuma na ukate shape uipendayo (hakikisha unakata vipande vinene kiasi na sio kama mandazi) Baada ya hapo ziweke sehemu yenye joto na uache ziumuke. Zikisha umuka zikaange katika moto mdogo ili ziive mpaka ndani. Zikisha iva zitoe na uziweke katika kitchen towel ili zichuje mafuta. Ziache zipoe na hapo zitakuwa tayari kwa kuliwa

Jumamosi, 27 Septemba 2014

JUICE YA UBUYU

Mahitaji
Ubuyu(wa unga au wa mbegu)
Maji
Sukari
Njia:
1.Chambua ubuyu,ondo uchafu wowote uliopo kwenye ubuyu
2.Katika sufuria,weka ubuyu kisha ongeza maji.Katika kila kipimo cha ubuyu ongeza maji mara tatu yake
Ubuyu wa mbegu vikombe 6  weka maji vikombe 9
Ubuyu wa unga  vikombe 3 weka maji vikombe 12
3.Funika sufuria kisha bandika jikoni,chemsha adi vitokote,vipe  angalau dakika nne za kutokotea.
 
Kumbuka maji unayotumia kuchemsha ubuyu ni maji ya bomba na si salama,hivyo ni muhim kuyapa  muda mzuri wa kuchemka ili juice yako iwe salama.
4.Juisiinapoanza tu kutokota ongeza sukari kwa ladha uipendayo kisha acha zile dakika nne za kutokota ziishe.Zima jiko acha juisi ipoe.
Napenda kuweka sukari ichemkie kwenye juice kwani inafanya juice ishikane na kua nzito.Sukari ikichemshwa inakawaida ya kua nzito.Kumbuka kwamba ubuyu ni mwepesi sana na juice yake kawaida hujitenga inapotulia,ubuyu waenda chini na maji yanabaki juu.Ukichemsha sukari inasaidia kuondoa hali hiyo.
5.Chuja juisi,ongeza maji kama unaona ni nzito sana,na ongeza sukari endapo ile uliyoweka awali haitoshi.Juisi tayari kwa kunywa

Pilau Ya Nyama Ya Ng'ombe Na Nyanya






Vipimo

Mchele (Basmati)                                          3 vikombe

Nyama ya ngo’mbe                                      1 kg

Pilipili boga                                                    1 kubwa

Nyanya                                                        2 kubwa

Vitunguu maji                                               2 vikubwa

Kitunguu saumu(thomu/galic) iliyosagwa       1 kijiko cha supu

Tangawizi                                                     1 kijiko cha chai

Ndimu                                                          1

Mafuta ya kupikia                                         ½ kikombe

Mdalasini                                                      ½  kijiko cha chai

Binzari nyembamba                                      1 kijiko cha chai

Pilipili manga                                                  ½ Kijiko cha chai

Hiliki                                                             ½ Kijiko cha chai


Namna ya kutayarisha na Kupika


Roweka mchele wako katika chombo


Chukuwa nyama na ioshe vizuri na itie thomu, tangawizi, ndimu, pilipili manga na chumvi kiasi


Iweke jikoni hadi ikauke maji na kuwa imewiva huku ukiikaanga kaanga kwa hayo hayo mafuta yake hadi kuwa rangi ya hudhurungi


katakata Vitunguu na nyanya weka pembeni


Chukua pilipili boga, thomu, tangawizi na visage katika mashine ya kusagia


Weka sufuria pembeni na utie mafuta, subiri yapate moto


Kisha tia vitunguu na vikaange hadi kuwa hudhurungi na tia nyanya


Kisha mimina mchanganyiko wako ulio usaga wa pilipili boga, thomu na tangawizi


Koroga kwa dakika kadhaa Kisha mininia nyama uliyokuwa tayari, maji kiasi na chumvi wastani na subiri maji hayo yachemke


Weka mchele humo na koroga kiasi na onja chumvi kama ipo sawa au kama ndogo unaweza kuongeza


Funika na punguza moto na uache uive taratibu


Baada ya kukauka maji kabisa basi ugeuze na subiri tena kwa dakika kama mbili na tayari kuliwa.

Jumatatu, 22 Septemba 2014

karibuniii

Karibuni katika blog yetu ya mapishi.Hapa mtajifunza mengi yahusuyo mapishi.